Biashara ya virutubisho lishe ni kubwa sana na inaendelea kukua.
Kwa mujibu wa makadirio ya Grand View Research, soko la dietary supplements duniani lilifikia takribani dola bilioni 209.5 mwaka 2025, na linatarajiwa kufikia karibu dola bilioni 393.6 ifikapo mwaka 2033, likiwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 8.1 kwa mwaka kati ya mwaka 2026 na 2033.
Virutubisho lishe vinapatikana katika aina mbalimbali, ikiwemo vidonge, kapsuli, unga na vinywaji, na hutumiwa kuongeza vitamini, madini au virutubisho vingine mwilini.
Nchini Tanzania, ingawa bado hakuna takwimu pana za kitaifa zinazoonyesha ni asilimia ngapi ya Watanzania wote wanaotumia virutubisho lishe, utafiti uliofanywa katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa matumizi ya bidhaa hizo yameenea miongoni mwa baadhi ya watu wazima katika mazingira ya mijini.
Utafiti huo ulifanywa na Mark Lwakatare na Jane Mlimbila, ukiwahusisha watu wazima 419 kutoka taasisi za umma na binafsi katika Wilaya ya Ilala. Utafiti huo ulichapishwa mwaka 2023 katika jarida la Health Services Insights.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa asilimia 46.5 ya washiriki walikuwa wametumia virutubisho lishe katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti.
Miongoni mwa virutubisho vilivyotumiwa, multivitamin viliongoza kwa asilimia 64.1, vikifuatiwa na virutubisho vya madini kwa asilimia 34.9, huku virutubisho vya mitishamba vikitumiwa na asilimia 26.7 ya washiriki.
Utafiti huo pia umebaini changamoto katika namna baadhi ya watu wanavyotumia bidhaa hizo, ambapo asilimia 35.9 ya watumiaji walisema walijiamulia kutumia virutubisho bila kupata ushauri wa mtaalamu wa afya.
Hali hii inaibua mjadala kuhusu usalama wa matumizi ya virutubisho, hasa wakati ambapo biashara hiyo inaendelea kukua kupitia maduka, mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya biashara mtandaoni.
Baadhi ya bidhaa hutangazwa kwa madai kwamba zinaweza kupunguza uzito kwa haraka, kuongeza nguvu za kiume, kuongeza kinga au hata kutibu magonjwa mbalimbali.
Wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza kuwa kirutubisho lishe hakipaswi kuchukuliwa moja kwa moja kama dawa ya kutibu ugonjwa, na kwamba si kila madai yanayotolewa kwenye matangazo yana ushahidi wa kutosha wa kisayansi.
Kimataifa, mamlaka za udhibiti zimewahi kutoa tahadhari kuhusu baadhi ya bidhaa za virutubisho, hususan zinazodai kusaidia kupunguza uzito au kuongeza nguvu za kiume, baada ya baadhi yao kubainika kuwa na viambato vya dawa ambavyo havijaelezwa kwenye lebo.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu wanashauri wananchi kuwa makini kabla ya kununua au kutumia virutubisho lishe, kusoma taarifa za bidhaa, kuangalia mtengenezaji, viambato, maelekezo ya matumizi na kuhakikisha bidhaa inakidhi matakwa ya mamlaka husika.
Aidha, mtu mwenye tatizo la kiafya anashauriwa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kabla ya kuanza kutumia virutubisho, hasa anapotumia dawa nyingine.
Kwa ujumla, ukuaji wa soko la virutubisho lishe unaonyesha kuwa bidhaa hizi zimekuwa sehemu ya biashara kubwa ya afya duniani. Hata hivyo, pamoja na fursa hiyo, kuna umuhimu wa kuongeza elimu kwa wananchi, kuimarisha udhibiti wa bidhaa na kukabiliana na matangazo yenye madai ya kupotosha ili kuhakikisha usalama wa watumiaji.
Na kwa Tanzania, watafiti wanaona umuhimu wa tafiti zaidi zinazoweza kutoa picha pana ya kitaifa kuhusu kiwango cha matumizi ya virutubisho lishe, aina zinazotumiwa, sababu za matumizi na changamoto zinazowakabili watumiaji.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni