Breaking


Alhamisi, 24 Septemba 2026

TAASISI ZA ELIMU YA JUU ZATAKIWA KUIMARISHA UTAFITI NA UBUNIFU

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (MB), amezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuimarisha tafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia ili kutoa suluhisho *la* changamoto zinazoikabili jamii na kuchangia maendeleo *ya* endelevu.

Masauni ametoa rai hiyo leo, Septemba 24, 2026, wakati akifunga rasmi Mkutano wa Tatu wa Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano (Five Universities Consortium), uliofanyika katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ya Afrika (NM-AIST), Arusha.

Amesema vyuo vikuu havipaswi kubaki kuwa vituo vya kuzalisha maarifa pekee, bali vinapaswa kuwa vitovu madhubuti vya utatuzi wa changamoto, kwa kuunganisha utafiti, sayansi, teknolojia, sera, sekta binafsi na mahitaji ya jamii.

“Mkutano wenye mafanikio haupaswi kuishia kwenye uwasilishaji wa mwisho au sherehe ya kufunga mkutano. Ninaamini kuwa katika siku hizi tatu za mkutano huu, mliibua maswali mapya ya utafiti, ushirikiano mpya, teknolojia mpya, mawazo mapya ya sera na uwekezaji, na hatimaye matokeo yanayoonekana na kupimika,” amesema.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo, “Kutoka Majadiliano hadi Matokeo Chanya: Kuunganisha Sayansi, Teknolojia, Sera na Ustahimilivu wa Hali ya Hewa kwa Ajili ya Mustakabali Endelevu,” ni ya wakati *muafaka* na inahitaji washiriki kugeuza mijadala na mawazo yaliyotolewa kuwa hatua na matokeo halisi.

Mhe. Masauni amewataka washiriki wa mkutano huo, hususan watafiti, wanasayansi na wabunifu vijana, kuhakikisha maarifa na uvumbuzi unaozalishwa katika taasisi za elimu na utafiti unafika katika jamii na kutatua changamoto halisi.


Amesema sayansi haiwezi kuwa na matokeo makubwa iwapo manufaa yake yatabaki ndani ya kuta za taasisi za utafiti na vyuo vikuu.

“Dunia inahitaji mawazo yenu. Msizuie malengo yenu kwenye matatizo yaliyo karibu nanyi tu. Anzeni na matatizo hayo, yaeleweni kwa kina, kisha jiulizeni ni kwa namna gani maarifa na suluhisho mnazozibuni zinaweza kuchangia maendeleo ya Afrika na dunia nzima,” amesema.

Aidha, amewataka washiriki kujiuliza ni ushirikiano gani mpya wa utafiti umeanzishwa kupitia mkutano huo, ni changamoto zipi zinaweza kutatuliwa kwa pamoja, na ni uvumbuzi gani unaweza kutoka maabara na kutumika katika jamii.

Waziri Masauni amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu katika kufikia maendeleo endelevu.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya utafiti na ubunifu, kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu na taasisi za utafiti, pamoja na kukuza ushirikiano na sekta binafsi na jumuiya ya kimataifa.


Kwa mujibu wa Masauni, ushahidi unaozalishwa kupitia tafiti za kisayansi unapaswa kutumika kwa ufanisi zaidi katika kuandaa na kuboresha sera za umma. Muungano wa huo unashirikisha Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Aga Khan, SUA pamoja na Chuo Kikuu cha Simon Fraser (SFU).


Pia amesisitiza umuhimu wa mipango inayowaunganisha watafiti wa Tanzania na washirika wa kikanda na kimataifa, akisema hatua hiyo itasaidia kuzifanya taasisi za Tanzania kuwa wachangiaji hai katika uzalishaji wa maarifa ya kisayansi duniani.

Hakuna maoni: