Serikali imesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango nchini, ikieleza huduma hizo ni sehemu muhimu ya uwekezaji katika afya, ustawi wa jamii na maendeleo ya rasilimali watu kuelekea kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 28, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Bi. Ziada Sela, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani, yaliyowakutanisha viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi, vyama vya kitaaluma pamoja na vijana.
Amesema uzazi wa mpango unatoa fursa kwa familia kufanya maamuzi sahihi kuhusu idadi ya watoto na nafasi baina ya mtoto mmoja na mwingine, huku ukisaidia kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kuchangia kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo la tatu linalohusu afya bora na ustawi.
“Ahadi ya Tanzania Family Planning 2030 inatoa msingi muhimu wa kuimarisha ufadhili endelevu wa ndani kwa ajili ya uzazi wa mpango, ikiwemo kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya bidhaa za uzazi wa mpango kwa angalau asilimia 10 kila mwaka na kuhakikisha fedha zinazotengwa zinatolewa kikamilifu,” amesema Bi. Sela.
Naye, Naibu mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Bi. Melissa McNeil-Barrett amesisitiza uzazi wa mpango hauhusiani tu na upatikanaji wa bidhaa na huduma, bali pia kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, wanafikiwa na huduma hizo na wanakuwa na uhuru wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Aidha, amepongeza hatua zinazochukuliwa na serikali ya Tanzania katika kuimarisha uongozi na kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani kugharamia huduma, bidhaa za uzazi wa mpango na huduma nyingine za afya ya uzazi.
Katika maadhimisho hayo, yaliyoambatana na midahalo, mawasilisho na hoja mbalimbali, wadau wametakiwa kuendelea kushirikiana kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utekelezaji wa afua za uzazi wa mpango katika ngazi zote, ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kuchangia kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni