Tanzania na Japan zimeazimia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika kukuza na kutangaza utalii baina ya nchi hizo mbili.
Hayo yamejiri leo Septemba 25 wakati Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Mamlaka ya Utalii Japan (Japan Tourism Agency) Norio Kimura kwenye mkutano wa pembezoni katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Japan (Tourism Expo Japan 2026) yanayoendelea Tokyo nchini humo.
Katika mazungumzo hayo Waziri Kijaji amesema Tanzania ina utajiri wa vivutio vikiwemo vya wanyamapori, hifadhi za misitu na malikale ambavyo vikitangazwa kikamilifu vitawavutia watalii wengi kutoka Japan, miongoni mwa maeneo ya ushirikiano yaliyojadiliwa ni pamoja na uendelezaji wa mazao ya utalii, utangazaji utalii, uwekezaji katika sekta za utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya watalii wanaosafiri kati ya nchi hizo mbili.
Waziri Kijaji amesema Tanzania ipo tayari kupata uzoefu kutoka Japan juu ya nammna bora ya kutumia teknolojia katika kukuza na kutangaza utalii kupitia programu maalumu alizozipendekeza za kubadilshana uzoefu ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo baina ya wataalamu wa Tanzania na Japan.
Mkutano huo uliofanyika Kwa mafanikio makubwa ukiweka azimio la utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kukuza na kutangaza Utalii kwa ushirikiano baina ya Japan Tourism Agency na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Mapema Kabla ya mkutano huo Waziri Kijaji alitembelea Mabanda ya nchi mbalimbali likiwemo banda la taasisi na wadau wa utalii kutoka Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Japan na kuzungumza na baadhi ya wadau na washiriki katika maonesho hayo akiwasisitiza juu ya kuongeza ubunifu katika kutangaza utalii kupitia maonesho haya.
Amesema taasisi na wadau wanaopata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika maonesho ya kimataifa wanatakiwa kufanya maonesho yanayoakisi ubora na upekee wa vivutio vinavyopatikana Tanzania ili kuvutia wengi kutembelea Tanzania na hapo ndipo ushiriki katika maonesho utakuwa na tija.









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni