Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema Tanzania itaendelea kuweka kipaumbele katika kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa, bidhaa za afya na vifaa tiba, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje, kuimarisha usalama wa afya nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Mchengerwa amesema hayo jijini New York, Marekani, wakati akizungumza katika kikao cha ‘Sustaining Sierra Leone’s Triple Zero Gains Through 2028’, ambapo ameiwakilisha Tanzania akiambatana na Katibu Mkuu, Dokta Grace Magembe, katika mjadala kuhusu namna ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana Sierra Leone katika kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kuongeza huduma za chanjo.
Kikao hiki ambacho kimeratibiwa na Serikali ya Sierra Leone, kinafanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kikao cha 81 (UNGA 81), unaowakutanisha wawakilishi wa nchi zote 193 wanachama wa UN na kila nchi ina kura moja ambapo kwa Tanzania, Makamo wa Rais, Deogratius Ndejembi, anamwakilisha Rais, Dokta Rais Samia Suluhu kuongoza ujumbe wa Tanzania.
Akizungumza katika mkutano huo, Mchengerwa, amefafanua kuwa Tanzania inaunga mkono kikamilifu Mpango wa Umoja wa Afrika wa AU Champion Roadmap 2026–2030 unaolenga kufikia malengo ‘zero tatu’, ambayo ni kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani na usio na wataalamu, kutokuwepo kwa vifo vya mama na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika, pamoja na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo.
“Tanzania inajivunia kuwa na Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika ajenda hii. Chini ya uongozi wake, tunaunga mkono kikamilifu AU Champion Roadmap 2026–2030 na Zero tatu,” amesisitiza Mchengerwa.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni