Breaking


Jumatano, 14 Oktoba 2026

DC MUHEZA AONGOZA SIKU YA PROTINI TANGA

Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Ayubu Sebabili amewaongoza watumishi wa Taasisi zote za Umma na wananchi waliopo kwenye Maonesho ya Wiki ya Chakula Duniani yanayoendelea mkoani Tanga kuadhimisha siku ya Protini iliyoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Taasisi zake.

Mhe. Sebabili ameipongeza Wizara kwa hatua hiyo ambayo ameeleza kuwa inaendelea kuwa chachu ya wananchi kuongeza ulaji wa mazao yatokanayo na sekta za Mifugo na Uvuvi.

“Siku hii sio tu inahamasisha ulaji wa nyama, samaki na unywaji wa maziwa bali ni darasa kwa wananchi juu ya namna ya kuandaa vyakula vya protini itokanayo na wanyama na samaki kwa sababu hata maandalizi yake na muonekano ni tofauti na tunavyoona huko mtaani” Amesema Mhe. Sebabili.

Awali wakati akimkaribisha Mhe. Sebabili, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Taifa ya Uvuvi Dkt. Ofred Mhongole amesema kuwa tukio hilo sehemu ya mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Wizara hiyo katika kuongeza kiwango cha ulaji wa protini itokanayo na wanyama na samaki ambapo amewataka wananchi wote kutumia jukwaa hilo kufahamu mambo yote yanayohusu vyakula hivyo.




Siku ya Protini huadhimishwa kando ya Maonesho ya Wiki ya Chakula Duniani ambapo wananchi na wadau wote hupata fursa ya kula vyakula vya protini itokanayo na wanyama na samaki huku kivutio kikubwa kikiwa ni mitindo mbalimbali inayotumika kuandaa vyakula hivyo.

Hakuna maoni: