Na MWANDISHI WETU
WANAFUNZI wanaotarajia kuhitimu elimu ya sekondari ya kidato cha nne wametakiwa kuzingatia nidhamu, kujituma na kutumia vizuri muda wao kufikia malengo ya kitaaluma na kutimiza ndoto zao za maisha.
Wito huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Climate Action Network Tanzania (CAN Tanzania), Dk. Sixbert Mwanga katika Mahafali ya 20 ya Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful.
Dk. Mwanga alisema nidhamu, bidii katika masomo na matumizi mazuri ya muda ni mambo muhimu yanayoweza kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao na kujiandaa kwa hatua zinazofuata za maisha.
Katika mahafali hayo, aliahidi kuchangia sh. milioni mbili kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano, sawa na jumla ya sh. milioni 10, kusaidia wanafunzi wenye changamoto za kifedha kupitia Taasisi ya Revival Education Trust.
Alisema msaada huo unalenga kuunga mkono juhudi za kuhakikisha watoto wanaotoka katika familia zenye changamoto za kiuchumi wanapata fursa ya kuendelea na masomo badala ya kukatiza safari yao ya elimu kwa kukosa fedha.
Dk. Mwanga alisema uamuzi wake wa kuchangia elimu umetokana na uzoefu wake wa maisha, akieleza kuwa safari ya elimu inaweza kukabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini msaada kutoka kwa wazazi, jamii na wadau wengine unaweza kumwezesha mwanafunzi kufikia malengo yake.
Alibainisha kuwa baada ya kumaliza masomo yake, alipata ufadhili uliomwezesha kuendelea na elimu nchini Afrika Kusini na Ujerumani, hatua iliyomsaidia kuongeza maarifa na baadaye kupata ajira.
“Nipo tayari kushirikiana na Taasisi ya Revival Education Trust kuimarisha shughuli zake iweze kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji,” alisema.
Alisisitiza umuhimu wa taasisi zinazosaidia elimu kuendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotambulika, pamoja na kuweka mifumo imara ya kuhakikisha misaada inayotolewa inawafikia walengwa na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Aidha, aliutaka uongozi wa shule hiyo kutathmini mahitaji ya sasa ya elimu na kuweka mikakati ya kupanua huduma zake kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi na jamii, bila kuathiri ubora wa elimu inayotolewa.
Kwa upande wake, Muasisi wa Shule ya Sekondari Huria ya Ukonga Skillful, Diodorus Tabaro, alisema shule hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Revival Education Trust imepanga kusaidia wanafunzi 100 wenye changamoto za kifedha waweze kurejea shuleni na kuendelea na masomo yao mwaka ujao.
Alisema mpango huo unalenga kuwasaidia watoto walioacha masomo kutokana na changamoto za kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua fursa za elimu na kuwawezesha kutimiza ndoto zao.
Tabaro alisema ushirikiano huo ni muhimu katika kuwafikia wanafunzi wenye uhitaji na kuwapa nafasi nyingine ya kuendelea na masomo yao, licha ya changamoto zinazokabili familia zao.
Alieleza kuwa kuwasaidia watoto kurejea shuleni ni hatua muhimu katika kuhakikisha changamoto za kifedha haziwi kikwazo cha kupata elimu na kujenga maisha bora ya baadaye.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni