NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Hamad Hassan Chande (Mb) ameshiriki Mkutano wa 13 wa Baraza la Kisekta la Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliohudhuriwa na Mawaziri wa nchi za jumuiya hiyo.
Mkutano huo uliofanyika Jijini Arusha umeazimia kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika Sekta ya Utalii na Usimamizi wa Wanyamapori, sambamba na kuoanisha sera, mifumo ya udhibiti, masharti ya utoaji wa leseni na viwango vya ubora wa huduma za kitalii na kuitangaza Afrika Mashariki kama kituo kimoja cha utalii, ili kuongeza ushindani katika soko la dunia.
Aidha, mkutano huo umeweka mikakati ya pamoja ya kukuza utalii endelevu, kuboresha ubora wa huduma na kuongeza manufaa ya kiuchumi yatokanayo na rasilimali za utalii zilizopo kwenye nchi za jumuiya hiyo.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, amesema kuwa mafanikio ya Sekta ya Utalii hayategemei mvuto wa rasilimali zilizopo EAC pekee, bali ubora wa huduma zinazotolewa, uzoefu wanaopata wageni na ushirikiano wa nchi wanachama katika kuitangaza Afrika Mashariki kama eneo moja la utalii.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Makame akiambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Chande, Naibu Waziri wa Utalii na Malikale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Hassan Thabit (Mb), na watendaji waandamizi kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni