Breaking


Jumanne, 6 Oktoba 2026

KAMISHNA WA UHIFADHI TANAPA AFANYA ZIARA SERENGETI

 


Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Massana Mwishawa leo Oktoba 05, 2026 amefanya ziara ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika hifadhi hiyo na kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji ambazo miradi hiyo imefikia ikiwa ni sehemu ya kuendelea kusimamia maendeleo na uboreshaji wa miundombinu ya uhifadhi na utalii ndani ya hifadhi.

Miradi iliyokaguliwa ni pamoja na mradi wa Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti “Serengeti National Park Golf Course”, ambao umekamilika kwa kiwango kikubwa na unatarajiwa kuzinduliwa katikati ya mwezi Oktoba 2026; matengenezo ya Kituo cha Kuongozea Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Seronera; Kituo cha Kutolea Taarifa kwa Wageni cha Serengeti (Serengeti Visitor Center) kilichojengwa chini ya ufadhili wa Serikali ya Ujerumani ambacho kinatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 07, 2026; pamoja na Daraja la Viboko lililopo katika barabara ya Seronera - Naabi





Matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja itasaidia kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii sambamba na kupunguza athari katika msimu wa mvua El Niño. Ziara hiyo ilimuhusisha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Godwell Meng’ataki, ambaye ndiye Mkuu wa Kanda ya Magharibi, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ismail Ismail ambaye ndiye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Hakuna maoni: