Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imepokea ujumbe kutoka mashirika mawili ya Serikali ya Korea Kusini, Korea International Cooperation Agency (KOICA) na Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH), waliofika kujadili namna ya kuimarisha huduma za dharura na ajali nchini, hususan mfumo wa huduma za dharura za kitabibu (EMS).
Ujumbe huo umetembelea Idara ya Dharura na Ajali ya hospitali hiyo, ambapo umejionea huduma zinazotolewa pamoja na juhudi zinazoendelea za kuokoa maisha ya wagonjwa.
Mkuu wa Idara ya Dharura na Ajali, Dkt. Nanyori J. Lucumay, amesema ushirikiano huo utasaidia kuboresha mfumo wa EMS na kuongeza upatikanaji wa magari ya dharura, hatua itakayopunguza muda wa kuwafikisha wagonjwa hospitalini.
Amesema idara hiyo inapokea wagonjwa wenye uhitaji wa huduma za haraka, wakiwemo wa kiharusi, kisukari, majeruhi wa ajali na wenye changamoto za mfumo wa fahamu, ambao watanufaika kwa kupata huduma stahiki kwa wakati, hivyo kuongeza fursa ya kuokoa maisha na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni