Aliyekuwa Rais wa Senegal, Macky Sall, amejiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa iliyotolewa mjini Marrakesh, Morocco, Sall amesema amefikia uamuzi huo kufuatia kura ya maoni isiyo rasmi iliyofanyika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 16 Oktoba, pamoja na mazungumzo aliyofanya na marais wawili waliounga mkono azma yake: Évariste Ndayishimiye wa Burundi na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal.
Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, ambaye kwa sasa anaongoza Umoja wa Afrika-AU, ndiye aliyependekeza jina la Sall kwa nafasi hiyo.
Sall amesema ameamua kujiondoa kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, ili kusaidia kuhakikisha kuwa mgombea atakayechaguliwa anapata uungwaji mkono mpana kutoka kwa pande mbalimbali.
Amesema kura ya majaribio iliyofanyika kwa siri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilionyesha kuwa nchi nyingi zinaunga mkono nafasi hiyo kupewa mgombea kutoka Amerika ya Kusini na Karibiani.
Pia ametoa wito wa kufanyika kwa mageuzi makubwa ndani ya Umoja wa Mataifa ili kuipa Afrika nafasi kubwa zaidi katika kufanya maamuzi yanayohusu masuala ya kimataifa.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni