Breaking


Ijumaa, 9 Oktoba 2026

MKAMA AAGIZA POSTA KUBORESHA HUDUMA KWA TEKNOLOJIA


Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Mkama, amelitaka Shirika la Posta Tanzania na wadau wa sekta hiyo kuwekeza katika teknolojia za kisasa, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji wa nyaraka na vifurushi, pamoja na kuongeza ubora wa huduma ili kukidhi mahitaji ya wateja. Amesema sekta ya posta inapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa biashara mtandao kwa kutoa huduma za haraka, nafuu na salama.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yenye kaulimbiu isemayo “Mtandao Mmoja wa Posta, Uwezeshaji Usio na Kikomo,” Dkt. Mkama amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria yatakayochochea uwekezaji, ushindani na ubunifu katika sekta hiyo.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kidijitali inayowawezesha wateja kufuatilia nyaraka na vifurushi vyao katika hatua zote za usafirishaji, huku ikilinda usalama, faragha na taarifa za wateja. Amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa huduma na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kutumia biashara mtandao kufikia masoko ya ndani na kimataifa.

Aidha, ameitaka sekta ya posta kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote, wakiwemo wanaoishi vijijini na maeneo yenye changamoto za kibiashara. Ameeleza pia umuhimu wa kuendeleza Mfumo wa Kitaifa wa Anwani za Makazi, ambao utarahisisha usafirishaji wa vifurushi, bidhaa na utoaji wa huduma nyingine za kijamii na Serikali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia sekta ya posta ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kulindwa haki zao. Amewahimiza wananchi kutumia huduma za watoa huduma wenye leseni za TCRA na kutoa taarifa wanapokumbana na changamoto ili kusaidia kuboresha huduma hizo.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Posta Tanzania, Ferdinand Kabyemela, aliyemwakilisha Postamasta Mkuu, amesema shirika hilo linaendelea kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya uandishi wa barua kwa wanafunzi kwa lengo la kukuza ujuzi wa lugha na mawasiliano. Amesema mwaka huu zaidi ya wanafunzi elfu moja kutoka shule za msingi na sekondari walishiriki mashindano hayo, wakiwemo wavulana zaidi ya mia tatu na wasichana zaidi ya mia nane.







Ametoa wito kwa wananchi, wafanyabiashara na wadau kuendelea kutumia huduma za Shirika la Posta Tanzania, akieleza kuwa uwekezaji katika teknolojia na ushirikiano ni muhimu katika kujenga sekta ya posta yenye ushindani na ufanisi. Amesema hatua hizo zitasaidia kupanua fursa za biashara, kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Hakuna maoni: