Breaking


Jumatatu, 26 Oktoba 2026

MNH-MLOGANZILA YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI KWA WATOTO WENYE KICHWA KIKUBWA NA MGONGO WAZI

Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imeendelea kuimarisha huduma za matibabu na upasuaji kwa watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi, ambapo katika kipindi cha miaka minne iliyopita, watoto 4,000 wamepatiwa huduma za afya na 600 kufanyiwa upasuaji hospitalini hapo.


Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Upasuaji Dkt. Godlove Mfuko wakati alizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH katika Maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi yaliyoandaliwa na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHT), yaliyofanyika MNH-Mloganzila.


Dkt. Mfuko amesema hospitali imeendelea kuongeza uwezo wa kutoa huduma hizo kupitia upatikanaji wa wataalamu bingwa, akiwemo mtaalamu wa ubingwa wa juu aliyebobea katika upasuaji wa mfumo wa fahamu kwa watoto kupitia ufadhili wa Samia Health Super Specialization Program .


Ameongeza kuwa MNH-Mloganzila ina mpango wa kuwa Kituo cha Umahiri katika upasuaji wa mfumo wa fahamu kwa watoto, sambamba na kutenga chumba maalumu kwa ajili ya upasuaji wa watoto kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma. 


Aidha, amesisitiza kuwa hospitali inalenga kuhakikisha watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi wanaohitaji upasuaji wanapata huduma hiyo ndani ya saa 48 baada ya kufika hospitalini hapo, kulingana na tathmini ya hali zao za kiafya.


Akizungumzia umuhimu wa kinga, Dkt. Mfuko amewahimiza wanawake wanaopanga kupata ujauzito na wajawazito kutumia madini ya foliki (folic acid) kwa ushauri wa wataalamu wa afya, kwani husaidia kupunguza hatari ya mtoto kuzaliwa na changamoto za ukuaji wa mfumo wa fahamu, ikiwemo mgongo wazi. 


Pia amesisitiza umuhimu wa bima ya afya kwa wote katika kupunguza vikwazo vya kifedha na kusaidia mwendelezo wa matibabu.


Maadhimisho hayo yamewakutanisha watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na muongo wazi, familia zao kutoka mikoa mbalimbali, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuimarisha huduma, ushauri wa kitaalamu na elimu kwa jamii kuhusu kinga, matibabu, malezi na ustawi wa watoto hao.



Hakuna maoni: