Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za usingizi ganzi nchini kwa kuongeza wataalamu, vifaa tiba na fursa za mafunzo ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma salama wakati wa upasuaji.
Prof. Sunguya ameyasema hayo Oktoba 17, 2026, alipomwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Mohammed Mchengerwa katika Marathon ya hisani ya Run for Patient Safety 2026, iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wataalamu wa Usingizi Ganzi Tanzania kwa lengo la kuhamasisha usalama wa wagonjwa na kuchangisha fedha kwa ajili ya ununuzi wa mashine 150 za ufuatiliaji wa hali za wagonjwa (portable monitors), hususan katika vituo vya afya vya maeneo yenye changamoto.
Amesema wataalamu wa usingizi ganzi wana nafasi muhimu katika kulinda maisha ya wagonjwa wakati wa upasuaji kwa kufuatilia upumuaji, mapigo ya moyo na hali zao kwa ujumla, akieleza kuwa mchango wa kada hiyo mara nyingi hauonekani licha ya kuwa na umuhimu mkubwa katika kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji.
“Bila ninyi hakuna tiba salama, hakuna upasuaji salama. Tunawaona na tunawatambua,” amesema Prof. Sunguya, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya madaktari wa usingizi ganzi, madaktari wa upasuaji, wakunga na wataalamu wengine wa afya katika kuimarisha huduma za uzazi salama.
Prof. Sunguya ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuimarisha mafunzo ya wataalamu wa kada hiyo kupitia programu mbalimbali, ikiwemo Samia Scholarship, huku ikichukua hatua za kuongeza idadi ya wataalamu bingwa na wabobezi ili kukabiliana na upungufu wa watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Aidha, amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba, kuhakikisha mashine za ufuatiliaji wa wagonjwa zinafanya kazi katika Hospitali za Wilaya na kuimarisha vyumba vya uangalizi wa wagonjwa baada ya upasuaji.
Ameongeza kuwa Wizara itafanyia kazi suala la uwakilishi wa wataalamu wa usingizi ganzi katika ngazi za maamuzi ili kuhakikisha mahitaji ya kada hiyo yanazingatiwa katika mipango ya sekta ya afya nchini.
Prof. Sunguya amewataka wataalamu wa afya na wanariadha walioshiriki marathon hiyo kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu usalama wa huduma za upasuaji na umuhimu wa huduma bora za usingizi ganzi, akisisitiza kuwa juhudi za kulinda maisha ya wagonjwa zinahitaji ushirikiano wa kila siku ndani na nje ya vyumba vya upasuaji.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni