
Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha, kujenga uwezo wa kitaasisi na kuendeleza miradi ya uhifadhi wa bioanuwai na mazingira nchini.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha miradi inayopendekezwa inaandaliwa kwa ubora unaostahili, inakidhi vigezo vya ufadhili na inatekelezwa kwa ufanisi na uendelevu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu na Mwenyekiti wa GEF, Diego Mesa Puyo, pembezoni mwa Mkutano wa 17 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Hifadhi ya Bioanuai, uliofanyika jijini Yerevan, Armenia, Oktoba 28, 2026.
Katika mazungumzo hayo, Tanzania imependekeza kuanzishwa kwa majadiliano ya kitaalamu kati ya GEF, Ofisi ya Makamu wa Rais na taasisi husika za kisekta, ikiwemo taasisi zinazotekeleza miradi, ili kubaini mahitaji ya kifedha na kuweka vipaumbele vya uwekezaji katika uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Tanzania imeiomba GEF kutoa mwongozo kuhusu namna ya kuoanisha miradi inayopendekezwa na mwelekeo wa programu za mfuko huo, vigezo vya kustahili ufadhili pamoja na taratibu zinazopaswa kufuatwa katika hatua za maandalizi na utekelezaji wa miradi.
Katika kuimarisha upatikanaji wa rasilimali fedha, Tanzania pia imependekeza kuwepo kwa mikakati ya pamoja ya kuhamasisha fedha kutoka Serikalini, kwa washirika wa maendeleo, mashirika ya uhifadhi na sekta binafsi inayowajibika.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa vyanzo vya fedha na kuongeza uwezo wa kugharamia miradi ya uhifadhi wa bioanuwai na mazingira kwa muda mrefu.
Vilevile, Tanzania imehimiza majadiliano kuhusu mifumo endelevu ya ufadhili wa uhifadhi, ikiwemo uanzishwaji wa mifuko ya dhamana ya uhifadhi, malipo kwa huduma za mifumo ikolojia na uwekezaji unaochangia uhifadhi wa mazingira, huku ukizingatia ulinzi wa mazingira na maslahi ya jamii.
Katika hatua nyingine, Tanzania imeiomba GEF kuongeza msaada wa kitaalamu na kitaasisi kwa Ofisi ya Uratibu ya Kituo cha Kitaifa cha Uendeshaji wa GEF nchini ili kuimarisha uwezo wake wa kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili na kutekelezwa kwa ufanisi.
Msaada huo unatarajiwa kujumuisha maandalizi ya miradi, ukusanyaji wa takwimu za msingi, tafiti za upembuzi yakinifu na uandaaji wa maandiko ya awali ya miradi yaliyo tayari kwa uwekezaji.
Kwa ujumla, hatua hizo zinalenga kuimarisha uratibu kati ya taasisi za Serikali na wadau wa maendeleo, kuongeza upatikanaji wa fedha na kujenga uwezo wa kitaasisi ili kuhakikisha miradi ya uhifadhi wa bioanuwai nchini inaandaliwa kwa viwango vinavyohitajika na kupata fursa pana zaidi za ufadhili.
Kupitia ushirikiano huo, Tanzania inalenga kuimarisha juhudi za uhifadhi wa bioanuwai na mazingira kwa kuhakikisha uwekezaji katika sekta hiyo unakuwa endelevu na unazingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni