Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço, wameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Ushirikiano wa Huduma za Usafiri wa Anga baina ya Nchi Mbili (BASA), uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam, tarehe 29 Oktoba 2026.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa mkataba huo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema:
*“Mkataba huu utawezesha uwepo wa safari za moja kwa moja kati ya nchi zetu na hivyo kuchochea biashara na shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwemo utalii. Kwa sasa, wasafiri kutoka Tanzania kwenda Angola hulazimika kupitia nchi nyingine, kama Ethiopia au Afrika Kusini. Tunataka kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Angola.”*
Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Mhe. Téte António.
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Dkt. Jabiri K. Bakari, walikuwa miongoni mwa viongozi walioshiriki katika hafla hiyo, inayolenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Angola katika sekta ya usafiri wa anga.
Mkataba wa BASA unaweka mfumo wa kisheria na kiutendaji wa kuwezesha ushirikiano wa huduma za usafiri wa anga baina ya nchi hizo mbili kwa mujibu wa masharti yaliyokubaliwa na pande husika. Kuwepo kwa safari za moja kwa moja kunatarajiwa kurahisisha usafiri wa abiria na kukuza fursa za biashara, uwekezaji na utalii kati ya Tanzania na Angola.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni