Wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya mambo ya nje ushirikiano wa afrika mashariki, Wizara ya Afya Zanzibar, pamoja na wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya wamekutana leo katika Ofisi za Wizara ya Afya, Mtumba jijini Dodoma, kupitia michoro ya usanifu wa kina na nyaraka za zabuni za ujenzi wa Makao Makuu ya Tume ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki (EAHRC).
Kikao hicho kinalenga kutathmini mahitaji ya kiufundi ya mradi huo, kujenga uelewa wa pamoja na kuandaa msimamo wa Tanzania utakaowasilishwa katika Mkutano wa Wataalamu wa Kikanda (RESC).
Akizungumza Oktoba 22,2026 Jijini Dodoma kuhusu umuhimu wa kikao hicho, Daktari Bingwa wa magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya Dkt. Michael Kiremeji amesema, Mapitio hayo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa maoni ya kitaalamu ya Tanzania yanazingatiwa na maandalizi ya ujenzi yanafuata viwango na taratibu zinazokubalika.
Dkt.Kiremeji amesema kikao hicho ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa katika mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 1 hadi 6, 2026, ambapo EAHRC, kwa kushirikiana na nchi wanachama, ilielekezwa kupitia michoro ya usanifu na nyaraka za zabuni za mradi huo.
Aidha,amesisitiza Mapitio hayo yanatoa fursa kwa wataalamu kujadili masuala ya kiufundi na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha maandalizi ya mradi, huku yakizingatia mahitaji ya utekelezaji na ushirikiano wa nchi wanachama.
Dkt.Kiremeji amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato huo, msimamo na mapendekezo ya Tanzania yatawasilishwa katika Mkutano wa Wataalamu wa Kikanda (RESC), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika utafiti wa afya na kuwezesha hatua zinazofuata za ujenzi wa Makao Makuu ya tume ya utafiti wa Afya katika nchi za Afrik mashariki (EAHRC).






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni