Usimamizi wa Akili Unde kwa Vyombo vya Habari ni mada iliyowakutanisha waandishi wa habari, wahariri na viongozi wa vyumba vya habari katika mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Tech & Media Convergency (TMC), kuanzia Oktoba 27 hadi 29, 2026, kjijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wanahabari kutumia teknolojia ya Akili Unde, kwa kuzingatia sheria, maadili na uwajibikaji katika shughuli za uandishi na uhariri wa habari.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo, washiriki walijadili mifumo ya kisheria na kisera inayohusiana na matumizi ya Akili Unde nchini Tanzania na Kenya.
Majadiliano hayo yaliongozwa na Wakili Robert Sylivester Majige, Kiongozi wa Sera na Teknolojia za Kiraia wa TMC, ambaye pia alielekeza washiriki kuhusu namna ya kubadilisha misingi ya usimamizi wa teknolojia hiyo kuwa kanuni na sera zinazotekelezeka katika vyumba vya habari.
Katika siku ya pili, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation TMF, Dastan Kamanzi, aliongoza majadiliano kuhusu hatua za kiufundi za kuhakikisha matumizi salama na yenye uwajibikaji wa Akili Unde.
Washiriki pia walibadilishana uzoefu kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo na kujadili maeneo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuandaa sera za vyombo vya habari.
Shughuli hizo zilifanyika chini ya usimamizi wa Anuar Said, mkufunzi na mshauri wa TMC, huku Janet John Kahindi, Mratibu wa Sera na Programu wa TMC, akiratibu maandalizi ya kazi za vikundi na uandishi wa rasimu za sera.
Katika siku ya mwisho ya mafunzo, leo Oktoba 29, washiriki ambao ni waandishi wa habari wamepitia rasimu ya sera ya matumizi ya Akili Unde na kutoa mapendekezo yao kwa lengo la kuiboresha na kuhakikisha inakidhi mahitaji halisi ya vyumba vya habari.
Mapendekezo hayo yanalenga kusaidia taasisi za habari kuwa na mwongozo utakaosimamia matumizi ya teknolojia hiyo kwa kuzingatia usahihi wa taarifa, maadili ya uandishi wa habari, uhuru wa uhariri, ulinzi wa taarifa binafsi na uwajibikaji.
Kupitia warsha hiyo, TMC inalenga kuimarisha uwezo wa taasisi za habari kutumia Akili Unde kwa uwajibikaji, huku zikilinda uadilifu wa uandishi wa habari na kuendeleza imani ya wananchi kwa vyombo vya habari katika mazingira ya kidijitali.













Hakuna maoni:
Chapisha Maoni