Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewahimiza vijana kutumia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri pamoja na fursa nyingine za kiuchumi zilizopo ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa wakati wa mkusanyiko wa michezo ya Jogging uliohusisha viongozi na wanachama wa vilabu mbalimbali pamoja na washiriki,
Akizungumza katika tukio hilo, Mpogolo amesema mikusanyiko ya michezo ni fursa muhimu ya kuimarisha umoja, mshikamano, upendo na mahusiano mema miongoni mwa wananchi, huku ikitumika pia kuhamasisha vijana kuhusu fursa za maendeleo na namna ya kujikwamua kiuchumi.
Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali na Halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wao, wakiwemo viongozi wa vilabu vya michezo, ili kutambua fursa zilizopo na kuzitumia kuboresha maisha yao. Aidha.
Mpogolo amewataka viongozi wa vilabu kuingiza ajenda za uwezeshaji kiuchumi katika vikao vyao na kushirikiana na uongozi wa Wilaya na Halmashauri kutafuta njia za kuimarisha uchumi wa vilabu na wanachama wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, amewahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kwenye kliniki za mafunzo kuhusu mikopo ya asilimia 10 ili kupata elimu ya taratibu za kusajili vikundi, kuandaa maombi na kutimiza vigezo vinavyohitajika ili kunufaika na mikopo hiyo.
Mabelya amesema zaidi ya Shilingi bilioni 20 zinapatikana kwa ajili ya mikopo hiyo, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni