Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma-PIC, imeitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania-TADB, kuimarisha mikakati ya kutafuta vyanzo mbadala vya mitaji ili kuongeza uwezo wake wa kutoa mikopo kwa wakulima wengi zaidi na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salam, na Mwenyekiti wa PIC, Ojambi Masaburi, wakati wa ziara ya Kamati katika benki hiyo, iliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, yenye jukumu la kusimamia uwekezaji wa Serikali katika taasisi na kampuni za umma.
Masaburi, amesisitiza umuhimu wa benki hiyo kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali kwa kutumia njia mbalimbali za kuongeza mtaji, ikiwemo utoaji wa hisa, hati fungani na kuingia katika ubia wa kimkakati.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kaimu Msajili wa Hazina, Lightness Mauki, amesema Serikali itaendelea kuiunga mkono TADB kwa kuimarisha mtaji wake, kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kuongeza uwezo wa benki hiyo kutekeleza majukumu yake.
Awali, akiwasilisha taarifa ya benki hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TADB, David Nghambi, amesema mtaji wa wanahisa wa benki hiyo umeongezeka kutoka shilingi bilioni-76.7 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi bilioni-553.2 mwezi Septemba mwaka huu 2026.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni