Breaking

Jumamosi, 12 Julai 2025

DKT. MPANGO AAGIZA KUONGEZA JITIHADA MAPAMBANO YA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA NA YASIYOAMBUKIZA.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo kwa Wizara za Kisekta ikiwemo Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuongeza  jitihada katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Dkt. Mpango amesema hayo leo Julai 12, 2025 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri ulioratibiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Dkt. Mpango amesema  kuna umuhimu mkubwa wa  kukabiliana na  Magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

"Ili kuimarisha huduma za Sekta ya Afya, nasisitiza udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kwa kuhakikisha jamii inakuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara, kufanya mazoezi , uondoaji  wa maji taka ,usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu," amesema Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango ameagiza elimu ya afya kuhusu matumizi sahihi ya dawa iendelee kutolewa ili kulinda afya ya jamii.

"Dawa zikitumika vibaya madhara ni makubwa kama vile matatizo ya figo, hivyo elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa ni muhimu, " amesema.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Sekta ya Afya imechagiza kwa kiasi kikubwa katika mapambano ya magonjwa ya kuambukiza.

"Katika kukabiana na magonjwa ya kuambukiza, sekta ya afya imechagiza kwa kiwango kikubwa , hii ni kutokana na uwekezaji Mkubwa wa Serikali kwenye sekta hii muhimu,” amesema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka jitihada kubwa katika kuhakikisha Afya ya Msingi inaimarika ili  kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya.

Akisoma risala kwa niaba ya Waganga Wakuu wa Mikoa, Mwenyekiti wa Waganga Wakuu wa Mikoa Dkt. Best Magoma ambaye pia ni Mganga Mkuu Mkoa wa Morogoro ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Udhibiti wa magonjwa ya mlipuko  ikiwemo Marburg na Mpox.

Hakuna maoni: