Breaking

Jumamosi, 12 Julai 2025

WAAJIRI WAHIMIZWA KUTUNZA KUMBUKUMBU ZA WATUMISHI KURAHISISHA UTOAJI WA MAFAO.


Waajiri wanatakiwa kutunza kumbukumbu za Watumishi wao kuanzia mtumishi anapoajiriwa hadi  anapofikisha muda wake wa kustaafu ili kusaidia katika utoaji wa mafao kwa wakati kwa mtumishi anapostaafu. 

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam  na Mhasibu Mwandamizi kutoka Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bi. Macelina Haule, alipokuwa akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Bi. Haule alisema kuwa, Waajiri wanawajibika kuwaelimisha watumishi wanaotarajia kustaafu kuhusu utaratibu wa malipo ya mafao, mafao atakayopata na Mfuko ambao atastahili kulipiwa baada ya kustaafu. 

“Watumishi nao wanawajibu wa kutunza nyaraka muhimu za utumishi wao zitakazosaidia wakati wa kuandaa mafao iwapo jalada la mwajiri litakuwa na nyaraka pungufu”, alisema Bi. Haule. 

Alisema kuwa wajibu wa Waajiri kwa wastaafu wanaohudumiwa na Hazina ni pamoja na  kukusanya majalada yote ya mstaafu kuanzia alipoanza kazi hadi anastaafu na kuhakikisha nyaraka muhimu zimo na kuyawasilisha Hazina.

Bi. Haule alitaja majukumu mengine kuwa ni pamoja na kufanya ukokotoaji wa malipo ya mafao, kuandaa hati ya Pensheni na kuwasilisha majalada yenye hati za pensheni kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aidha, alisema kuwa Waajiri wanatakiwa kupokea nyaraka muhimu za mirathi kutoka kwa ndugu wa marehemu na kuziwasilisha Hazina kwa ajili ya malipo.

Hakuna maoni: