Breaking

Jumapili, 13 Julai 2025

HIMIZENI JAMII KUZINGATIA MISINGI YA MAADILI-WAZIRI MKUU


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini nchini kuendelea kuihimiza jamii kuzingatia msingi ya maadili na kuepuka mienendo iliyo kinyume na tamaduni, mila na desturi ya Mtanzania.

Amesema kuwa moja ya eneo ambalo viongozi hao wanapaswa kukemea ni kuhusu  matumizi, biashara na usambazaji wa dawa za kulevya kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kunusuru maisha ya Watanzania hususan vijana.

Amesema hayo leo (Jumapili, Julai 13, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kumweka wakfu na kumuingiza kazini Askofu Mteule Dkt. Daniel Henry Mono wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

“Tuendelee kupambana vikali na matumizi ya dawa za kulevya sababu athari yake ni kubwa hasa kwa vijana wetu, vijana ni kundi tegemewa, matumizi ya dawa za kulevya yanaharibu uelewa na afya za vijana wetu”

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kwa upande wake imeendelea kuweka sheria kali pamoja na kuimarisha ukaguzi wa kubaini uingizaji wa dawa za kulevya nchini. “Tupo imara usikubali kushiriki katika biashara hii”.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameyapongeza madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuihudumia jamii ya Watanzania.

 


“Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini katika kufanikisha masuala mbalimbali yanayounganisha Taifa letu ikiwemo Agenda za kitaifa, kuimarisha masuala ya maadili na kujenga jamii inayozingatia misingi ya kudumisha upendo, amani na utulivu”

Ameongeza kuwa madhehebu hayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika kutoa huduma za afya, elimu, malezi ya vijana, utunzaji wa mazingira pamoja na huduma kwa makundi maalum yenye uhitaji ikiwa ni kuinga mkono Serikali katika kutoa huduma. 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali wakati wote itaendelea kufanya kazi na kushirikiana na madhehebu ya dini nchini kwa ajili ya manufaa ya watanzania wote.

Hakuna maoni: