Breaking


Jumapili, 27 Julai 2025

PROFESA MKENDA AZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA.


WAZIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Adolf Mkenda,amezindua wiki tatu za maadhimisho ya miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW)tangu kuanzishwa kwake na kuanza kutekeleza majukumu ya kutoa elimu ya kujiendeleza na mafunzo ya elimu ya watu wazima nchini mwaka 1975.

Maadhimisho hayo yanalenga kuangazia umuhimu mkubwa wa kujua kusoma na kuandika na kuendelea kujifunza bila ukomo.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 27,Mwaka huu Jijini Dodoma,Profesa Mkenda amesema kilele cha maadhimisho hayo kitatanguliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kongamano la siku tatu litakalofunguliwa na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan.

“Wadau wa elimu na wananchi zaidi ya 1,000 kutoka ndani nan je ya nchi watakutana katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam,kujadili masuala ya elimu bila ukomo,na litafungwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dokta Doto Biteko,”amesema.

Amesema kongamano hilo litashirikisha wadau mbalimbali wa elimu takribani 1,000 kutoka ndani nan je ya nchi ili kutafakari miaka 50 ya utekelezaji wa dhima na dira ya TEWW na mwelekeo wa elimu bila ukomo.

Maadhimisho hayo yamebeba kauli mbiu isemayo Elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu yakiwa yanalenga kuhusisha kasi ya wadau wa kitaifa na kimataifa ya kuendeleza elimu ya watu wazima nchini na kuongeza uelewa wa umma kwamba elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.



Hakuna maoni: