Breaking


Jumapili, 3 Agosti 2025

JAJI MWAMBEGELE ASISITIZA UMUHIMU WA MAUDHUI SAHIHI KUHAMASISHA USHIRIKI KATIKA UCHAGUZI 2025

 

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, akizungumza katika Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume hiyo na Wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Mkutano huo umefanyika leo, Jumapili Agosti 3, 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha washiriki mbalimbali wakiwemo mabloga (bloggers), watayarishaji wa video mtandaoni (YouTubers), na wachoraji wa katuni za kijamii.


Akizungumza katika mkutano huo, Jaji Mwambegele amesisitiza umuhimu wa maudhui sahihi, yenye kuelimisha na kuchochea ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia. Aidha, amewataka wazalishaji wa maudhui kutumia majukwaa yao kwa kuwahamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao. 

“Nawasisitiza na kuwakumbusha juu ya umuhimu wa kuepuka matumizi mabaya ya akili mnemba (Artificial Intelligence), ambayo kwa sasa inatumiwa na baadhi ya watu wenye nia ovu kusambaza taarifa za upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina matumaini makubwa na vyombo vya habari katika kuhakikisha mafanikio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia mchango wao wa kutoa taarifa sahihi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi.

“Imani hii inachochewa na ushirikiano wenu wa karibu mliouonesha tangu awamu za awali, hususan katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambapo mmekuwa mstari wa mbele kuwasilisha hoja, mapendekezo na ushauri kila tunapokutana kwenye vikao,” 




Kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni “Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura”, ikiwa ni wito mahsusi kwa kila raia mwenye sifa ya kupiga kura kuhakikisha anatimiza wajibu huo wa kikatiba.


Hakuna maoni: