Breaking

Ijumaa, 3 Oktoba 2025

KONGAMANO LA 12 LA AFYA KUANGAZIA TEKNOLOJIA NA TAKWIMU

Kongamano la 12 la Afya Tanzania (Tanzania Health Summit – THS 2025) limeanza leo katika Ukumbi wa Mkomazi, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, likiwa na mada kuu “Kutumia Takwimu na Teknolojia za NCDs Kuongeza Kasi ya UHC katika Huduma za Afya za Msingi nchini Tanzania.”

Kongamano hilo limewaleta pamoja wataalamu na wadau wa sekta ya afya kujadili namna takwimu na teknolojia zinavyoweza kubadilisha mfumo wa usimamizi wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuharakisha utekelezaji wa bima ya afya kwa wote (UHC).

Miongoni mwa wazungumzaji wakuu ni Prof. Kaushik Ramaiya, Lusajo Ndgile, Happy Nchimbi, Dk. Amani Kikula, Dk. Josephat Kamugisha na Dk. Rachel Nungu, ambao wanatarajiwa kutoa mitazamo na uzoefu katika kuunganisha teknolojia na takwimu kwenye utoaji huduma za afya za msingi.

Majadiliano ya mwaka huu yamekusudia kutoa dira na mikakati madhubuti itakayowezesha Tanzania kusonga mbele katika mapambano dhidi ya NCDs sambamba na jitihada za kufanikisha afya bora kwa kila Mtanzania.

Kongamano hili ni sehemu ya jukwaa la kitaifa la wadau wa afya ambalo limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuimarisha ushirikiano, ubunifu na ubadilishanaji wa uzoefu katika sekta ya afya.

Hakuna maoni: