Ujauzito kwa mwanamke mwenye ugonjwa wa seli mundu (sikoseli) huambatana na hatari kubwa kwa afya ya mama na mtoto, lakini haimaanishi kuwa hawezi kupata mtoto mwenye afya njema.
Kwa mujibu wa Dkt. Jamila Makame, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu kutoka Hospitali ya Amana, wanawake wengi wenye sikoseli wamefanikiwa kupitia ujauzito salama kwa msaada wa kitaalamu na matunzo ya karibu.
Akitolea ufafanuzi juu ya ugonjwa huo kwa mama mjamzito mwenye Sikoseli, kwa waandishi wa habari mjini Kibaha, Dkt. Jamila anafafanua, mama mjamzito mwenye sikoseli yuko kwenye hatari ya kupata upungufu mkubwa wa damu, maumivu ya kifua, kifafa cha mimba (pre-eclampsia), kuganda kwa damu, kujifungua mapema ama mtoto njiti.
Anasema, wakati wa ujauzito, mama anapaswa kuhudhuria kliniki kwa ukaribu kila wiki 4 hadi wiki ya 24, na kila wiki 1 hadi 2 hadi atakapojifungua kwa uangalizi wa kitaalamu.
Dkt. Pius Muzzazzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, anasema hakuna madhara kwa mama mwenye sikoseli kunyonyesha, na mtoto anaweza kupimwa wiki moja baada ya kuzaliwa.
Muzzazzi anabainisha, takwimu zinaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi tano zenye wagonjwa wengi, ambapo watoto takriban 14,000 huzaliwa na sikoseli kila mwaka, na ugonjwa huo unachangia vifo vya asilimia 7 ya watoto chini ya miaka mitano.
Nae Asteria Mpoto kutoka Wizara ya Afya sikoseli amesema, Sikoseli ni ugonjwa wa kurithi unaotokana na mabadiliko katika jeni ya hemoglobini, ambao huathiri uwezo wa chembe nyekundu kubeba oksijeni ili mtoto azaliwe na ugonjwa kamili, lazima arithi jeni kutoka kwa wazazi wote wawili.
Mwamvua Mwinyi-Kibaha




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni