Kikao kazi kati ya Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO, na viongozi wa Serikali za Mitaa kutoka manispaa za Ilala, Temeke na Kigamboni, kimefanyika leo jijini Dar es Salaam. Lengo la kikao hicho ni kujadili changamoto za upatikanaji wa umeme, kuboresha huduma, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya TANESCO na wananchi kupitia viongozi wao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amesema ushirikiano kati ya TANESCO na viongozi wa mitaa ni muhimu katika kutatua matatizo ya umeme kwa wakati. Amesisitiza kuwa viongozi wa mitaa na madiwani ndio kiunganishi kikuu kati ya wananchi na taasisi za huduma, hivyo kuwezesha taarifa za changamoto kuwafikia TANESCO haraka na kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji Lazaro Twange , amesema shirika hilo linaendelea kuongeza jitihada katika kuboresha huduma kwa wananchi, sambamba na maelekezo ya Serikali. Amesema kufanya kazi kwa karibu na viongozi wa mitaa kutarahisisha utoaji wa huduma bora, wa haraka na wenye uhakika.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Feri, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mwinamno, ameipongeza TANESCO kwa kuandaa kikao kazi hicho. Amesema kikao hicho kitawawezesha viongozi kwenda kutoa elimu zaidi kwa wananchi juu ya masuala ya nishati ya umeme na manufaa yake katika maendeleo ya kila siku.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni