Bondia maarufu wa ngumi za kulipwa, Ibrahim Mafia, anatarajiwa kurejea rasmi ulingoni tarehe 31 Desemba ndani ya mashindano ya KNOCKOUT YA MAMA Season 7, pambano linalotarajiwa kuwa la aina yake kutokana na ukubwa wa jina lake na maandalizi aliyoyafanya.
Mafia, anayejulikana kwa nidhamu, nguvu na moyo wa chuma, amesema kuwa pambano hilo si la kawaida bali ni fursa ya kuthibitisha ubora wake na heshima ya jina alilojijengea katika ulimwengu wa ngumi za kulipwa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mafia alisema kuwa amejipanga kikamilifu kimwili na kisaikolojia, huku akisisitiza kuwa anaingia ulingoni akiwa na dhamira moja tu ushindi.
“Hili ni pambano la heshima. Nimejiandaa kwa muda mrefu na nina uhakika wa kuonyesha uwezo wangu mbele ya Watanzania,” alisema Mafia kwa kujiamini.
Mashindano ya KNOCKOUT YA MAMA yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa mabondia wa ndani kuonyesha vipaji vyao, na msimu wa saba unatarajiwa kuvutia mashabiki wengi kutokana na mapambano makubwa yaliyopangwa, likiwemo hili la Ibrahim Mafia.
Wadadisi wa masuala ya michezo wanasema pambano hilo litakuwa jaribio muhimu kwa Mafia katika safari yake ya kuthibitisha ubingwa na kuandika historia mpya katika ndondi za Tanzania.
Mashabiki wa ngumi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo litakalojaa ushindani, nguvu na burudani ya hali ya juu.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni