Mdemu ametoa wito huo Desemba 15, 2025 wakati akizungumza na wanufaika wa mikopo hiyo akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma iliyolenga kukagua maendeleo ya vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Amewapongeza wanawake hao kwa maendeleo mazuri ya miradi yao, huku akiwakumbusha umuhimu wa kuendelea kurejesha mikopo kwa wakati."Urejeshaji mzuri wa mikopo ni msingi muhimu wa uendelevu wa mfuko huu wa WDF, kwani fedha hizi ni za mzunguko na zinalenga kuwainua wanawake wengi kiuchumi,hivyo tuhakikishe tunarejesha kwa wakati ili wanawake wenzetu nao waweze kunufaika nayo,"amesema.
Katika ziara hiyo, Mdemu amepata fursa ya kutembelea kikundi cha Five Dadas kinachojishughulisha na utengenezaji wa mikate, Kemmy Group kinachojihusisha na usindikaji wa vyakula na viungo kwa matumizi ya nyumbani, pamoja na mjasiriamali Neema Woisoo anayejihusisha na utengenezaji wa juisi na uendeshaji wa mgahawa wa chakula.
Katika maeneo hayo, amewapongeza kwa ubunifu na bidii waliyoionyesha katika kuendesha shughuli zao na kuwasisitiza kuongeza ubora wa bidhaa zao na kuzingatia upatikanaji wa masoko ili kukuza kipato chao na kuimarisha biashara zao.
Kwa upande wao, wajasiriamali walionufaika na mikopo hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mikopo hiyo wakisema imewasaidia kuanzisha na kupanua biashara zao, kuongeza kipato cha familia, kutoa ajira kwa wengine na kuboresha maisha yao kwa ujumla, hivyo kuchangia maendeleo ya jamii na Taifa.
"Tunaahidi kuendelea kusimama vyema biashara zao pamoja na kurejesha mikopo hiyo kwa wakati, ili kuwawezesha wanawake wengine wengi zaidi kunufaika na mfuko huo". amesema mmoja wa Mjasiriamali







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni