Breaking

Jumanne, 16 Desemba 2025

JAMII ISAIDIE WAFUNGWA VIFUNGO VYA NJE WASIRUDIE UHALIFU


 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, ameitaka jamii kufahamu kuwa ina wajibu wa kushirikiana na Serikali katika kurekebisha na kuwatunza wafungwa wanaotumikia vifungo vyao nje ya magereza, ili kuwazuia wasirudie kutenda uhalifu.

Gugu ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa kazi Idara ya Huduma ya Uangalizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kilicho husisha Viongozi wa Wafawidhi wa Mikoa

Ameeleza kuwa bado zipo changamoto za uelewa kuhusu dhana ya kifungo cha nje ya magereza, hivyo amewahimiza washiriki wa kikao hicho kuendelea kuelimisha jamii ili kila mmoja aelewe dhamira ya Serikali katika kusimamia utekelezaji wa adhabu hiyo mbadala.

Aidha, Gugu amesema kuwa adhabu mbadala husaidia kupunguza gharama za Serikali katika kuhudumia wafungwa, kupunguza msongamano magerezani, pamoja na kuwapa fursa wahalifu wa makosa madogo wenye sifa stahiki kufanya kazi za kijamii bila malipo kama njia mbadala ya kulipia makosa waliyoyafanya.



Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma ya Uangalizi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Nsanze, amesema kuwa marekebisho ya sheria yaliyoongeza muda wa adhabu kutoka miaka mitatu hadi minne yatawawezesha wafungwa wengi zaidi kupata fursa ya kutumikia kifungo cha nje ya magereza kama adhabu mbadala.

Hakuna maoni: