Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameagiza mafunzo ya kuwajengea weledi maofisa usafirishaji-Bodaboda kuhusu usalama barabarani na sheria za usafirishaji kutolewa mkoani humo.
Aidha, amezitaka mamlaka husika ikiwemo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kuhakikisha wahitimu wanapatiwa leseni baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo.
Kunenge ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo hayo kwa maafisa usafirishaji wa Wilaya ya Kisarawe yanayofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
Amesisitiza umuhimu wa maafisa hao kuwa wazalendo, kulinda amani ya nchi na kuwa mfano bora katika utendaji wao ili kuipa heshima Serikali na kumuenzi Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan.
Katika mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, ametoa rai kwa maofisa usafirishaji kuunda vikundi na kuvisajili mara baada ya kupata leseni ili kukidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya asilimia 10.
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Novemba 22, 2025 na kushirikisha maafisa usafirishaji 228, huku awamu ya pili ikihusisha washiriki 250.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni