Mfuko wa Misitu Tanzania (TAFF) umekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Chuo cha Viwanda vya Misitu (Forestry Industries Training Institute - FITI) kilichopo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza katika Mahafali ya 28 ya chuo hicho yaliyofanyika tarehe 5 Desemba 2025, Mtendaji Mkuu wa TAFF, Dkt. Tully Msuya, alisema kuwa fedha hizo zinalenga kujenga bweni la wasichana ili kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na kuongeza usalama na ustawi wa wanafunzi wa kike.
Aidha, katika hafla hiyo TAFF iliwakabidhi wanafunzi watatu walioweka rekodi ya ufaulu wa juu katika ngazi ya Astashahada mikataba ya ufadhili ili waweze kuendelea na masomo ya Stashahada ya Teknolojia ya Viwanda vya Misitu.
Ufadhili huo unajumuisha malipo ya gharama zote za chuoikiwemo ada, usajili, fedha za kujikimu na matumizi mengine muhimu ikiwa na jumla ya shilingi milioni 11.4 kwa wanafunzi wote watatu. Hatua hii inalenga kuongeza hamasa ya ufaulu na kuzalisha wataalam zaidi katika teknolojia ya viwanda vya misitu.
“Mfuko wa Misitu Tanzania una jukumu la kuboresha vyuo vya misitu na kuhakikisha vinatoa elimu bora inayoendana na mahitaji ya soko la ajira na utunzaji wa mazingira. Fedha hizi zitasaidia kupanua miundombinu ya FITI, na ufadhili huu unawawezesha wanafunzi kusoma bila kikwazo cha ukosefu wa fedha,” alisema Dkt. Msuya.
Dkt. Msuya aliongeza kuwa mfuko utaendelea kuvipatia vyuo vya misitu msaada unaohitajika hadi vitakapoweza kujitegemea katika miundombinu, ubunifu, na utoaji wa wahitimu wenye ujuzi utakaochangia maendeleo ya sekta ya misitu nchini.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni