Breaking


Jumapili, 14 Desemba 2025

ULEGA AKOSHWA NA MRADI WA BARABARA UNAOTEKELEZWA NA WANAWAKE


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa barabara ya Ruanda-Idiwili mkoani Songwe unaotekelezwa na wakandarasi wanawake waliopata fursa maalumu kutokana na maelekezo ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan.

Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilomita 20 na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni-45.3, wamepewa wanawake hao kupitia Umoja wa Wakandarasi Wanawake Tanzania ili kuonesha uwezo wao na kama wataifanya vizuri, watapewa pia miradi mingine.

Waziri Ulega amesema kwa muda mrefu wanawake walikuwa wakitumika zaidi katika shughuli za kusafisha barabara lakini Rais Samia ameamua kufanya uamuzi wa kimkakati ili wanawake sasa wafanye kazi kubwa zaidi na zenye kipato zaidi.

Waziri Ulega ambaye alikuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, ameeleza kufurahishwa na kasi yake aliwahakikishia kuwa Rais Samia anatambua mchango wa wakandarasi wanawake na ndio maana ameridhia kutoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kujenga barabara hiyo.

Aidha, amesisitiza suala la fursa za ajira kwa vijana wa eneo hilo ambalo mradi unatekelezwa na kufurahishwa na utoaji wa ajira kwa mradi huo kwa vijana na kuwataka kutolifanyia mchezo agizo hilo

Kwenye suala la uwezeshaji vijana katika ujenzi, Waziri Ulega, amesema msisitizo wa serikali ni kuhakikisha wanafanya kazi si za vibarua tu bali pia kupitia kampuni ndogo zinazoweza kupewa kazi za ujenzi. 

Aidha, amewataka Mameneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe na Mbeya, kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi hao na kutokuwepo kwa makosa madogo madogo ili ujenzi wa barabara hiyo uende kwa kasi na kukamilika kwa wakati uliokusudiwa.

Hakuna maoni: