Breaking


Ijumaa, 9 Januari 2026

𝐓𝐀𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈 𝐙𝐀 𝐔𝐌𝐌𝐀 𝐍𝐀 𝐁𝐈𝐍𝐀𝐅𝐒𝐈 𝐙𝐈𝐍𝐀𝐙𝐎𝐊𝐔𝐒𝐀𝐍𝐘𝐀 𝐍𝐀 𝐊𝐔𝐂𝐇𝐀𝐊𝐀𝐓𝐀 𝐓𝐀𝐀𝐑𝐈𝐅𝐀 𝐁𝐈𝐍𝐀𝐅𝐒𝐈 𝐙𝐈𝐉𝐈𝐒𝐀𝐉𝐈𝐋𝐈 𝐏𝐃𝐏𝐂 𝐊𝐀𝐁𝐋𝐀 𝐘𝐀 𝐀𝐏𝐑𝐈𝐋𝐈 𝟖, 𝟐𝟎𝟐𝟔 – 𝐌𝐇𝐄. 𝐊𝐀𝐈𝐑𝐔𝐊𝐈

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amezitaka taasisi zote za umma na binafsi zinazokusanya au kuchakata taarifa binafsi kuhakikisha zinajisajili Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kabla ya tarehe 8 Aprili, 2026.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya Maafisa wa Ulinzi wa Taarifa, Waziri Kairuki alisema Serikali imetoa kipindi cha nyongeza cha miezi mitatu kuanzia Januari 8, 2026 hadi Aprili 8, 2026, ili kutoa fursa ya mwisho kwa taasisi ambazo bado hazijatimiza matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kujisajili kwa hiari.

“Serikali imeamua kutoa muda huu wa ziada wa miezi mitatu kuanzia tarehe 8 Januari 2026 hadi tarehe 8 Aprili 2026, ili kuhakikisha hakuna taasisi inayokosa fursa ya kutekeleza wajibu wake wa kisheria. Baada ya tarehe hiyo, utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi utaanza kikamilifu bila msamaha wowote,” alisisitiza Mhe. Kairuki.

Aidha, Waziri aliielekeza Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kuanza mara moja maandalizi ya ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria, utakaoanza rasmi mara tu baada ya kumalizika kwa kipindi hicho cha nyongeza. Alisema ukaguzi huo utahusisha taasisi, kampuni na watu binafsi wote wanaokusanya, kuhifadhi au kuchakata taarifa binafsi.

“Taasisí au mtu yeyote atakayebainika kuendelea na shughuli za ukusanyaji au uchakataji wa taarifa binafsi bila kujisajili, au kinyume na matakwa ya Sheria na Kanuni zake, atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kusita,” alisema Waziri.

Wito huo unakuja katika juhudi za Serikali kuhakikisha haki ya faragha inalindwa, usalama wa taarifa binafsi unaimarishwa, na uwajibikaji katika matumizi ya taarifa za wananchi unazingatiwa ipasavyo katika sekta zote.



Hakuna maoni: