Klabu ya Esperance de Tunis imetoa wito mzito kwa mashabiki wake waliopo jijini Dar es Salaam, ikiwataka kuzingatia utulivu na nidhamu ya hali ya juu wakati wa mchezo wao dhidi ya Simba SC.
Kupitia taarifa rasmi, Esperance imewakumbusha mashabiki wake kuwa tayari imepokea onyo kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuhusu masuala ya kiusalama, ikisisitiza kuwa mashabiki wao hawaruhusiwi kuwasha vilipuzi au aina yoyote ya fataki uwanjani. Klabu imeonya kuwa ukiukwaji wa kanuni hizo unaweza kusababisha adhabu kali, ikiwemo kucheza mechi zijazo bila uwepo wa mashabiki.
Aidha, Esperance imeeleza kuwa licha ya kutokuwepo kwa taarifa rasmi kutoka Ubalozi wao kwa sasa, bado wanawahimiza mashabiki wao kushangilia kwa amani na kuepuka kujihusisha na vitendo vya vurugu au kujibu kwa namna yoyote iwapo watakumbana na changamoto au vitendo visivyofaa kutoka kwa mashabiki wengine.
Klabu hiyo imehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa nidhamu, uvumilivu na kuonyesha mfano mzuri wa ushabiki wa kiungwana katika mchezo huo muhimu.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni