Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amekutana na Rais wa Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF) Dkt. Patrice Motsepe, Jijini Rabat, Morocco na kukabidhi barua kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pamoja na kukabidhi barua hiyo, Makonda, aliyeongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amemhakikishia Dkt. Motsepe kuwa Rais Dkt.Samia yupo tayari wakati wote kushirikiana na CAF katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya kandanda ikiwemo mashindano mbalimbali.
Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maandalizi ya kuwa wenyeji wa AFCON 2027, sambamba na Kenya na Uganda na kwamba imedhamiria kuonesha tofauti kubwa na mashindano yaliyopita.
Kwa upande wake, Dkt. Motsepe amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kumuandikia barua na salamu zake za upendo na ushirikiano kwa CAF na amemhakikishia kuwa CAF ipo tayari kufanya kazi bega kwa bega na Tanzania ili kufikia maendeleo makubwa katika kandanda.
Aidha, Dkt.Motsepe ameelezea kufurahishwa na jitihada zilizofanywa na Rais Samia katika maendeleo ya mpira ikiwemo ujenzi wa miundombinu, kufanya mashindano ya CHAN 2024 kwa mafanikio na maandalizi mazuri yanayoendelea kuelekea AFCON 2027.
Motsepe ameahidi kuja Tanzania hivi karibuni kujionea maandalizi mbalimbali ya AFCON 2027 na kukutana na viongozi kwa mazungumzo.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni