Wakala ya Barabara za Vijini na Mijini (TARURA) Manispaa ya Morogoro imekamilisha ujenzi wa daraja la Fungafunga, daraja muhimu linalounganisha Kata ya Mji Mpya na Kata ya Kichangani, hatua inayotajwa kuwa mkombozi wa changamoto za muda mrefu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Kwa miaka mingi, wakazi wa kata hizo mbili walikabiliwa na usumbufu mkubwa hususan wakati wa msimu wa masika, ambapo eneo la Fungafunga lilikuwa likifurika maji na kusababisha kukwama kwa shughuli za kijamii na kiuchumi, ikiwemo usafiri, biashara na upatikanaji wa huduma muhimu.
Kukamilika kwa daraja hilo kumeleta ahueni kubwa, kikiimarisha mawasiliano kati ya kata hizo na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Wakazi wameeleza kuridhishwa kwao na mradi huo, wakipongeza TARURA kwa utekelezaji wa mradi wenye tija kwa jamii.
Aidha, wananchi wa Mji Mpya na Kichangani wameahidi kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo, ili idumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni