Breaking


Ijumaa, 6 Februari 2026

DKT. GRACE MAGEMBE AONGOZA DIPLOMASIA YA AFYA GENEVA, TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA UNITAID

 

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, ametumia vyema fursa ya Mkutano wa 158 wa Bodi Tendaji ya Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea jijini Geneva, Uswisi, kueleza jitihada na mikakati inayotekelezwa na Tanzania katika kuimarisha huduma za afya na kukuza uzalishaji wa bidhaa za afya zenye ubora.

Akizungumza leo Februari 06, 2026, pembezoni mwa mkutano huo, Dkt. Magembe amekutana na Mkurugenzi wa Programu wa Unitaid, Bwana Robert Matiru, ambapo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania, chini ya uongozi wa Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika kuweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji wa bidhaa za afya nchini.

Amesema kuwa Unitaid ni mdau muhimu katika safari ya Tanzania ya kuimarisha sekta ya afya, hasa kwa kuunganisha makampuni na utaalamu wa kimataifa, mabenki na fursa za mikopo nafuu, ili kuyawezesha kuanzisha na kuendeleza viwanda vya bidhaa za afya vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

“Tumetumia fursa hii kukutana na Unitaid kwa sababu linafanya kazi kwa karibu na makampuni duniani, kuyaunganisha na rasilimali na fursa zitakazowezesha uzalishaji wa bidhaa za afya zenye ubora na ushindani wa kimataifa,” amesema Dkt. Magembe.

Kwa upande wake, Bwana Robert Matiru amesema Unitaid itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha uwezo wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), ikiwemo kusaidia mchakato wa kupandishwa daraja kutoka ngazi ya tatu kwenda ngazi ya juu zaidi, hatua itakayoongeza uaminifu wa bidhaa za afya zinazozalishwa nchini.

Kikao hicho pia kimeazimia kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Unitaid, ambapo wadau wa Unitaid wameahidi kufika Tanzania kukutana na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya afya. Aidha, pande zote zimekubaliana kuteua wawakilishi wa mawasiliano (focal persons) ili kuharakisha utekelezaji wa makubaliano na kuhakikisha mafanikio ya ushirikiano huo kwa maslahi ya Watanzania.

Hakuna maoni: