Kuwasili kwa manowari ya kubeba ndege ya Marekani, USS Abraham Lincoln, katika eneo la operesheni la Kamandi ya Kati ya Marekani (CENTCOM) karibu na maji ya Iran, kumezua taharuki kubwa kimataifa na kuibua hofu ya uwezekano wa makabiliano makubwa ya kijeshi kati ya Washington na Tehran.
Hatua hii nyeti ya kijeshi inakuja katika kipindi ambacho Iran inapitia moja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yake ya hivi karibuni. Taifa hilo linakabiliwa na wimbi la maandamano ya wananchi yanayoendelea kushika kasi, huku kukiwa na madai ya mabadiliko ya kisiasa na kuangushwa kwa utawala uliopo. Maandamano hayo yameripotiwa kukandamizwa kwa nguvu kubwa, hali inayozidisha mvutano wa ndani.
Uwepo wa manowari hiyo yenye uwezo mkubwa wa kivita unaashiria ujumbe mzito wa Marekani, hatua ambayo wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanaiona kama ishara ya kujiandaa kwa hali yoyote itakayojitokeza. Hali hii inazidisha dhana kuwa uhusiano kati ya Marekani na Iran umefikia kiwango cha hatari zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka ya karibuni.
Kwa upande mwingine, viongozi wa Iran wanajikuta wakiwa chini ya shinikizo kubwa kutoka pande mbili ndani na nje ya nchi. Ndani, wanakabiliwa na wananchi waliokata tamaa na wanaoendelea kupaza sauti kudai mabadiliko, huku nje wakikabiliwa na rais wa Marekani ambaye ameacha msimamo wake ukiwa wa sintofahamu, jambo linaloongeza wasiwasi na taharuki katika uongozi wa Tehran.
Kwa hali ilivyo sasa, macho ya dunia yameelekezwa Mashariki ya Kati, huku swali kubwa likibaki: je, mvutano huu utaishia mezani kwa mazungumzo, au dunia inakaribia kushuhudia mgogoro mkubwa wa kijeshi?

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni