Breaking


Jumanne, 3 Februari 2026

ZAIDI YA WAGONJWA ELFU MBILI KUTOKA MALAWI KUTIBIWA TANZANIA, DIPLOMASIA YA TIBA UTALII YASHIKA KASI

 


Zaidi ya wagonjwa elfu mbili kutoka nchini Malawi wanatarajiwa kuwasili nchini Tanzania kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu, ikiwemo matibabu ya ugonjwa wa Saratani, hatua inayodhihirisha mafanikio ya Tanzania katika sekta ya afya barani Afrika.


Hatua hiyo inatokana na utekelezaji wa mkakati wa Diplomasia ya Tiba Utalii, unaolenga kuvutia wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali kuja kutibiwa nchini, kufuatia uwepo wa vifaa vya kisasa na bingwa vya matibabu vinavyokidhi viwango vya kimataifa.


Uwekezaji huo mkubwa katika sekta ya afya umetokana na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuimarisha miundombinu ya afya na ununuzi wa teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali.


Tayari, Serikali kupitia Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, imezindua rasmi mashine ya kisasa ya uchunguzi wa Saratani ya PET-CT Scan, pamoja na mfumo wa huduma ya miadi mtandaoni katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), jijini Dar es Salaam.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Mchengerwa amesema wagonjwa hao kutoka Malawi wanatarajiwa kuwasili nchini katika siku za hivi karibuni, huku Tanzania ikipanga kutumia ndege zake kuwachukua wagonjwa hao ili kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati na kwa urahisi.


Mashine ya PET-CT Scan yenye thamani ya shilingi bilioni 18.7, ina uwezo mkubwa wa kugundua Saratani mapema, kufuatilia maendeleo ya ugonjwa huo pamoja na kusaidia madaktari kupanga matibabu sahihi. Mashine hiyo inatarajiwa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 500 kila mwaka.


Kupatikana kwa huduma hiyo nchini kutapunguza kwa kiasi kikubwa gharama zilizokuwa zikiwalazimu wagonjwa kusafiri kwenda nje ya nchi, hususan India, ambako wastani wa gharama za kipimo hicho hufikia shilingi milioni 1.2 kwa mgonjwa mmoja.


Kutokana na maendeleo hayo, Serikali imewaalika Watanzania kutumia fursa hiyo adhimu kwa kufika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ili kupata huduma za kisasa za uchunguzi na matibabu.


Aidha, mbali na wagonjwa kutoka Malawi, Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha huduma za afya kwa wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Comoro, hali inayoendelea kuifanya nchi kung’ara kama kitovu cha tiba utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Hakuna maoni: