Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameweka wazi mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya ujenzi ndani ya siku 100 za kwanza za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku kwa mara ya kwanza akieleza hadharani maelekezo, vipaumbele na maono ya Rais kuhusu mustakabali wa sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza kuhusu tathmini ya siku 100 za kwanza tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, Waziri Ulega amesema kuwa mwelekeo, maono na vipaumbele vinavyotolewa na Rais Samia ndiyo msingi muhimu wa kutathmini kipindi hicho, kwani ndiyo yanayoamua kasi na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo serikalini.
Ulega aliyasema hayo katika mkutano uliofanyika eneo la King’ori, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ambapo alifafanua kuwa maelekezo makuu ya Rais katika sekta ya ujenzi ni pamoja na kukamilisha miradi yote iliyoanza, matumizi sahihi ya mali ya umma, kuimarisha uwajibikaji kazini, kupambana na uzembe pamoja na kutumia miundombinu ya ujenzi kama nyenzo ya kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Akitoa mifano na takwimu, Waziri Ulega alisema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 500 ndani ya siku 100 pekee kwa ajili ya kukarabati na kuboresha miundombinu ya ujenzi nchini, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya Rais Samia katika kuleta mapinduzi ya kweli kwenye sekta hiyo.
Aidha, alieleza kuwa eneo la King’ori lina umuhimu mkubwa kiuchumi na kimkakati kwa kuwa ni njia inayopitisha barabara kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na nchi jirani za Kenya na Uganda. Katika kuimarisha shughuli za usafiri na biashara, Serikali imeweka taa zaidi ya 200 katika eneo hilo ili kuongeza usalama, kupendezesha mazingira na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa saa 24.
Hatua hizo zinaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga miundombinu imara itakayochochea maendeleo ya uchumi na kuhakikisha Watanzania wanaishi maisha yenye utu na fursa zaidi za kiuchumi.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni