Breaking


Jumatatu, 9 Februari 2026

WAGONJWA WA KIFAAFA WAHITAJI MSAADA WA JAMII, SIO UNYANYAPAA

 

Wananchi wametakiwa kuacha mara moja vitendo vya unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kifafa na badala yake kuwajali, kuwaheshimu na kuwapa ushirikiano unaostahili. Imeelezwa kuwa unyanyapaa umekuwa chanzo kikubwa cha wagonjwa wengi wa kifafa kushindwa kupata msaada wa mapema kutoka kwa familia na jamii zinazowazunguka, hali inayosababisha kuchelewa kufika hospitalini na wengine kuwasili wakiwa katika hali mbaya kiafya.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani yaliyofanyika leo Februari 09, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Dkt. Samizi amesema Wizara ya Afya inaendelea kuandaa miongozo na taratibu mbalimbali zitakazosaidia kuhakikisha wagonjwa wa kifafa wanaishi katika mazingira salama, yenye heshima na staha, sambamba na kupata huduma bora za afya.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi, amesema kuwa unyanyapaa bado ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wa kifafa kutokana na imani potofu zilizojengeka katika baadhi ya jamii. Ameeleza kuwa bado wapo wanaoamini kifafa ni ugonjwa wa kurithi, laana au matokeo ya uchawi, jambo ambalo si la kweli kitaalamu.

Dkt. Magandi amesisitiza kuwa kifafa ni ugonjwa unaotibika na kudhibitika kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, hivyo jamii inapaswa kuachana kabisa na mila na dhana potofu, na badala yake kuwapa wagonjwa wa kifafa msaada, ulinzi na heshima wanayostahili kama binadamu wengine.



Naye Rais wa Chama cha Kifafa nchini, Profesa William Matuja, amesema elimu kwa jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya kifafa. Profesa Matuja amebainisha kuwa jamii ikielimishwa ipasavyo kuhusu ugonjwa huo, wagonjwa wengi watajitokeza mapema kupata matibabu, hali itakayowawezesha kuishi maisha ya kawaida, yenye tija na matumaini kama watu wengine wote.


Hakuna maoni: