Breaking


Jumamosi, 7 Februari 2026

MAONO YA RAIS SAMIA YAPASWA KUTAFSIRIWA KWA MATENDO – RC CHALAMILA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amewataka walimu na wadau wote wa elimu mkoani humo kuhakikisha wanatafsiri ipasavyo maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa vitendo ili kuinua kiwango cha elimu na kujenga kizazi chenye tija kwa taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na wadau wa elimu wa mkoa huo, wakiwemo walimu wakuu, maafisa elimu na viongozi mbalimbali wa sekta ya elimu, Mhe. Chalamila amesema Serikali ina matarajio makubwa na dira pana katika sekta ya elimu, jambo linalodhihirishwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa katika maeneo mbalimbali ya elimu nchini.

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unapaswa kuendana na matokeo chanya, kwa kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika masomo yao na kuhitimu wakiwa na maarifa na ujuzi utakaowafanya kuwa raia wenye mchango chanya kwa maendeleo ya taifa.

“Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye elimu, hivyo ni wajibu wa walimu na wadau wote kuhakikisha maono ya Rais yanatekelezwa kwa vitendo kupitia ufundishaji wenye ubora na malezi bora ya wanafunzi,” amesema RC Chalamila.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Elimu pamoja na Wakuu wa Idara za Elimu kushirikiana kwa karibu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu, ili kuwawezesha kutimiza malengo na maono ya Rais Samia katika sekta ya elimu.

Kwa upande wao, Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Gift Kyando, pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bw. Elihuruma Maberya, wamewasilisha hali halisi ya sekta ya elimu mkoani humo pamoja na mipango inayotekelezwa ili kuboresha utoaji wa elimu.

Viongozi hao pia wamezungumzia mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hususan kwa wanafunzi watakaomaliza darasa la saba na la sita mwaka ujao, ambapo wote wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028.

Sambamba na hilo, baadhi ya walimu walioshiriki mkutano huo wameiomba Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya shule, hasa miundombinu na upatikanaji wa madawati, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Hakuna maoni: