Breaking


Jumanne, 24 Februari 2026

MHE BALOZI OMAR: TANZANIA NA SINGAPORE KUKUZA ZAIDI USHIRIKIANO WA KIUCHUMI


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Tanzania iko tayari kushirikiana zaidi na Singapore katika sekta za kukuza uchumi kupitia sekta mbalimbali ikiwemo kukuza biashara na uwekezaji, utalii, matumizi ya akili unde (Artificial Intelligence) pamoja na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato ya Serikali kwa njia ya kidigitali.

Mhe. Balozi Omar ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Douglas Foo, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia. 

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa miongoni mwa masuala waliyojadili kwa kina ni pamoja na kuharakisha mchakato wa kukamilisha nyenzo za Mkataba wa kulinda biashara na uwekezaji lakini pia Mkataba wa kuzuia utozaji kodi mara mbili kati ya nchi hizo mbili.

Alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na Singapore ambapo amewaalika wawekezaji kutoka nchini humo kuja Tanzania ili kutumia fursa za soko la kikanda kutokana na jiografia ambapo nchi imekuwa lango kuu la biashara katika nchi zaidi ya sita zisizopakana na Bahari.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa Singapore imepiga hatua kubwa katika sekta ya matumizi ya kidigitali katika ukusanyaji kodi na kwamba Tanzania iko tayari kuvuna maarifa hayo ili kuboresha ukusanyaji Mapato yake Kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Singapore nchini Tanzania mwenye makazi yake nchini Singapore, Mhe. Douglas Foo, aliahidi kuwa Serikali yake iko tayari kushirikiana zaidi na Tanzania kwa kuyahamasisha mashirika na Kampuni za nchi hiyo kufanya biashara na kuwekeza mitaji na teknolojia nchini Tanzania.

Alisema kuwa Tanzania imekuwa mshirika mzuri wa Singapore tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa nchi hizo mbili miaka 46 iliyopita na kwamba ushirikiano huo unahitajika kuimarishwa zaidi kwa faida ya pande hizo mbili.

Hakuna maoni: