Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Mhe. CP Suzana S. Kaganda, akiambatana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, wameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki shughuli ya ukaribisho katika Mkutano wa Wiki ya Nishati Endelevu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika mjini Victoria Falls, nchini Zimbabwe.
Akifungua vikao vya awali vya mkutano huo, Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. July Moyo, aliwakaribisha washiriki wote na kuwataka kufanya maandalizi madhubuti kuelekea ufunguzi rasmi utakaofanyika Februari 25, 2026. Amesema mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Kuendeleza Ukuaji wa Uchumi wa Kikanda kupitia Nishati Safi na Matumizi Bora ya Nishati.”
Mkutano wa Wiki ya Nishati Endelevu wa SADC unawakutanisha mawaziri na wadau mbalimbali wa sekta ya nishati kutoka nchi wanachama kwa lengo la kujadili na kukuza fursa zilizopo katika nishati endelevu pamoja na programu zinazohusu mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha, mkutano huo unatarajiwa kujikita katika majadiliano kuhusu utekelezaji na usimamizi wa sera za nishati safi pamoja na matumizi bora ya nishati, ambapo unatarajiwa kuhitimishwa Februari 27, 2026, mjini Victoria Falls, Zimbabwe.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni