Wataalamu kutoka Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) cha Wizara ya Fedha, kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar kupitia Idara ya Mashirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPD), wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili maandalizi ya kikao cha kwanza cha ushirikiano kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha, ambapo wataalamu hao walijadili kwa kina masuala muhimu yanayohusu utekelezaji wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, ikiwemo kupitia na kuthibitisha ajenda zitakazojadiliwa katika Kikao cha Kwanza cha Ushirikiano kati ya pande hizo mbili.
Aidha, kikao hicho kilitumiwa pia kupitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyotokana na Kikao cha Pili cha Ushirikiano kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ili kutathmini hatua zilizofikiwa na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine, wataalamu hao walipata wasilisho kuhusu Rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi wa Misaada ya Kibajeti na Madeni Sanjari, ambao unalenga kuimarisha uwazi, ufanisi na usimamizi bora wa rasilimali katika miradi ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Mikutano hiyo inaendelea kuonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi kama nyenzo muhimu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni