WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ametoa taarifa kuwa wizara yake imetengewa Shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa Kampuni changa 50, hatua inayotekeleza moja ya ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alizoahidi kutekeleza ndani ya siku 100 za uongozi wake.
Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, Rais Samia aliahidi kutekeleza jumla ya ahadi 13 ndani ya siku 100, ambapo ahadi tatu zinaigusa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 4, 2026, Jijini Dodoma, Waziri Kairuki amesema fedha hizo zitasaidia biashara ndogo, za kati, na Kampuni changa, na zinaelekea kutolewa kupitia Benki za Biashara kwa Kampuni ambazo zitakidhi vigezo vilivyowekwa katika mwongozo wa utoaji wa mikopo.
Kampuni zinazohusiana na mpango huu zinashughulikia sekta mbalimbali ikiwemo: Fedha, Sheria, Kupanga Matukio, Afya, Akili Endelevu, Kilimo, Utalii, Bima, Elimu, na Lishe. Kwa sasa wizara ipo katika hatua ya kukamilisha makubaliano na Benki za Biashara, ili kuhakikisha Kampuni changa za TEHAMA zinapata mikopo yenye riba nafuu.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa uwezeshaji huu utawezesha kampuni changa kuongeza uwekezaji kwenye rasilimali watu na miundombinu, kuboresha ubora wa bidhaa na huduma, na pia kuimarisha usalama wa mifumo yao.
Hii ni hatua nyingine muhimu inayothibitisha kuwa ahadi za Rais Samia hazibaki kwenye maneno, bali zinafanikiwa kutekelezwa kwa vitendo na kuongeza ukuaji wa sekta ya teknolojia na biashara nchini.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni