Serikali imesema imesikia na kuchukua hatua baada ya kupokea barua ya mwanafunzi Mariana Eric Mirindima, wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani, aliyewasilisha kilio cha changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya mijini maarufu kama daladala.
Kupitia barua hiyo, Mariana alieleza kwa kina namna baadhi ya madereva na makondakta wanavyogoma kuwabeba wanafunzi kwa madai ya kibiashara, wakidai kuwa wanafunzi hawalipi nauli kamili. Hali hiyo imekuwa ikiwalazimu wanafunzi kusimama barabarani kwa muda mrefu wakisubiri usafiri, kuchelewa kufika shuleni, na wakati mwingine kushindwa kabisa kuhudhuria masomo.
Kutokana na changamoto hizo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ametoa maagizo matano muhimu kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ili kuhakikisha haki, usalama na ustawi wa wanafunzi zinalindwa.
Miongoni mwa maagizo hayo ni LATRA kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala, hususan nyakati za asubuhi na jioni, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri bila vikwazo.
Aidha, Waziri Mbarawa ameagiza kuharakishwa kwa zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili makondakta katika miji yote nchini, sambamba na kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria dhidi ya madereva au makondakta watakaobainika kuwanyanyasa au kuwanyima wanafunzi haki yao ya usafiri.
Agizo jingine ni kuimarishwa kwa udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya utoaji huduma pamoja na usalama wao wakati wote. Vilevile, LATRA imetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma za usafiri na watumiaji, ili kila upande ufahamu haki na wajibu wake.
Kadhalika, Waziri ameagiza kuhakikisha treni za abiria, daladala zote nchini pamoja na mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani, zinaandikwa namba za bure kwa ajili ya malalamiko, ili abiria waweze kuwasiliana moja kwa moja na LATRA kupitia 0800 11 00 19 au 0800 11 00 20 pale wanapokumbana na changamoto.
Serikali imesisitiza kuwa usalama wa wanafunzi ni jambo la kipaumbele, na kwamba hakuna mtu au kundi litakaloruhusiwa kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa kuwanyanyasa katika huduma za usafiri wa umma.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni