Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamejadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalam na kitaaluma kwa lengo la kuimarisha taaluma na sayansi ya hali ya hewa ili kuchangia katika kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.
Majadiliano hayo yamefanyika katika kikao maalum kilicholenga kuangalia maeneo ya ushirikiano uliopo na namna ya kuuboresha, hususan katika matumizi ya tafiti zinazofanywa na UDSM kuhusiana na masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, alieleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo umedumu kwa muda mrefu na kikao hicho kimeweka mkazo katika kuimarisha maeneo mahsusi ya ushirikiano huo, ikiwemo kuimarisha uelewa na matumizi ya akili mnemba (AI) katika utafiti na huduma za hali ya hewa.
Akiongea wakati wa uwasilishaji wake Dkt. Paul T. S. Limbu Mhadhiri Mwandamizi wa Meteorolojia na Sayansi ya Hali ya hewa katika Idara ya Fizikia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema kwa zaidi ya miaka 13 ya kufundisha masomo ya hali ya hewa, bado kuna haja ya kuendelea kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya UDSM na TMA.
Tunawashukuru sana TMA kwa kushiriki na kutusaidia katika mchakato wa kuboresha mitaala, ufundishaji na usimamizi wa tafiti.
Pia ameeleza umuhimu wa wanafunzi kupata elimu kwa vitendo kupitia ziara za kitaaluma katika miundombinu ya TMA, fursa za kujitolea baada ya kuhitimu, pamoja na ushiriki wa TMA katika uandaaji wa vitabu vya kufundishia .
Aidha, pande hizo zimejadili ushiriki wa UDSM katika warsha, semina na maadhimisho ya siku muhimu kama Siku ya Hali ya Hewa Duniani ili kuwajengea wanafunzi uzoefu wa moja kwa moja katika mazingira halisi ya kazi.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msingi wa kuendeleza mazungumzo ya kitaalam yatakayosaidia kuunganisha tafiti, elimu na utekelezaji katika kuboresha huduma za hali ya hewa nchini.



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni